UMUHIMU WA KUJIANDAA NA MAISHA YA NDOA

Katika kumuumba kwake mwanadamu, Mwenyezi Mungu aliweka utaratibu wa kuwepo mahusiano kati ya mume na mke, ili kuendeleza uzao kwa wanadamu, kuwaondolea upweke na kuwatunukia utulivu, faraja, huruma, mapenzi, upendo na ushirikiano.

“Na katika ishara zake ni kuwa amekuumbieni wake zenu kutokana na nafsi zenu ili mpate utulivu kwao. Naye amejaalia mapenzi na huruma baina yenu. Hakika katika haya bila ya shaka zipo ishara kwa watu wanaofikiri”. Arruum21.

Kutokana na Mwenyezi Mungu kuwajengea wanadamu mahusiano hayo ya jinsia mbili tofauti, aliweka sharti na utaratibu wa mahusiano hayo, nao ni utaratibu wa ndoa kati yao.

Kimsingi ndoa kwa wanadamu ni uhalalishaji adilifu wa mahusiano ya mume na mke.

Mahusiano ambayo yamewekewa utaratibu mahususi ya kukubalika nakutambulika rasmi.

Kusudio la kuwepo utaratibu huu wa ndoa ni kuweka mipaka ya kimahusiano miongoni mwa wanadamu na kuondoa vurugu za watu kuingiliana hovyo.

Hii ina maana ya kudhihirisha kwamba mke au Mume wa mtu anaheshimiwa kwakuwa kwake katika mafungamano ya ndoa.

Na atakayejaribu kuingilia mahusiano hayo ambayo yamekuwepo kwa utaratibu huo wa Mwenyezi Mungu, huyo anatizamwa kuwa hayawani, mwasherati, mzinzi na asiye na utu.

Mwenyezi Mungu anaeleza katika Qur’an, “Na Allah (sw) amekuumbieni wake katika jinsi yenu, na akakujaalieni kutoka kwa wake zenu wana na wajukuu, na akakuruzukuni vitu vizuri vizuri.

Basi je, wanaamini upotovu na wanazikataa neema za Allah?”

“Mwenye kufunga ndoa (atakuwa) amekamilisha nusu ya Imani (dini yake) na amuogope Allah katika nusu itakayobakia” Ameisahihisha Sheikh Albaani katika Silsila Sahihi.

Kutokana na umuhimu wa ndoa katika maisha ya mwanadamu, tumeona kuna haja ya kukumbushana, hasa vijana jinsi ya kujiandaa na maisha ya ndoa kabla ya kuona.

Katika Uislamu inapofikia hatua ya kutaka kuoa au kuolewa, pande zote mbili hukabiliwa na mawazo mengi ni vipi atampata mchumba sahihi.

Tatizo kubwa ni katika kumchagua mwenza sahihi na mwenye sifa, ambaye utakapompata na kumuoa/kuolewa, atakuwa ndiye mshirika wako wa maisha.

Vile vile hutizamwa ni vigezo gani atumie muoaji au muolewa katika kufikia lengo lake la kumpata anayestahili na kukidhi.

Ikumbukwe kwamba pamoja na kwamba kuna dhana kwamba mwanamke hawezi kuchumbia na hana nafasi ya kuchagua mume anayetaka aolewe naye, lakini ukweli ni kwamba kwa utashi wake mwanamke ana haki ya kumkubali au kumkataa mchumba anayekuja kwake.

Kwa ujumla mambo ya ndoa huwasumbua watarajiwa huku kila mmoja akiwa na mitazamo tofauti katika chaguo.

Kila upande ukiwa umekua na kulelewa katika mazoea, desturi na tamaduni tofauti, mambo ambayo yana athari kwa namna moja au nyingine katika makuzi.

Baadhi ya wenye dhamira ya kuoa au kuolewa, wanakuwa hawafahamu wanahitaji mke au mume wa aina gani. Wakati mwingine wanajikuta wanaingia katika hamu ya kuwa katika ndoa, lakini bila kujua wanataka kuwa na wenza wa namna gani.

Wengine hujikuta wakijiingiza katika ndoa bila ya kuwa na ufahamu wa kutosha au taaluma yoyote inayohusiana na maisha hayo ya mahusiano na hatimayake hukosa uwezo wa kuziendesha ndoa zao.

Lakini pia wapo ambao hawana kabisa uelewa wa misingi ya kuoa na kuolewa zaidi ya kusukumwa na fikra finyu ya kutamani kuwa na mwenza kwa ajili ya kukidhi tu matamanio ya nafsi na hususan tendo la ndoa na kurahisishiwa baadhi ya majukumu kama vile kupika, usafi wa nyumba, kufua nk.

Wapo wanaotamani kuingia katika mahusiano ya ndoa kwa lengo moja tu,la kupata wepesi wa kupata mali na maisha ya anasa na starehe.

Kwa ujumla wengi wanaotaka kuoa au kuolewa, mara nyingi hawana fikra halisi na pana ya kusudio la ndoa.

Si kidini wala si kimazingira.

Hata maandalizi katika kuliendea jambo hilo wakati mwingine hayafanyiki vya kutosha na kwa kiasi kikubwa.

Uchaguzi wao hautizami sekta za msingi kama dini na maadili kwa ujumla wake.

Siku hizi sehemu kubwa ya jamii yetu imezoea kuyafanya masuala ya ndoa kuwa ni mambo ya kiutamaduni na si masuala ya kidini kama inavyotakikana.

Ndio maana hata kipaumbele katika hizo ndoa huwekwa zaidi katika masuala ya kijamii na kitamaduni na dini ikiwekwa pembeni kama sifa ya ziada.

Kwa mtazamo huo, ndoa nyingi zimekosa uvumilivu na kuendelea kuporomoka na kusababisha utengano wa kifamilia na magomvi kwa kasi ya kutisha.

Matokeo yake, badala ya kuunganisha familia kama ilivyokusudiawa na kujenga udugu, ndoa zimekuwa chachu ya utengano wa kifamilia, kuporomoka udugu na kuwa chanzo cha huduma mbovu za kijamii katika familia na wanaoathirika zaidi ni watoto.

Katika kufanya uchaguzi wa mtarajiwa, iwe ni mume au mke,kuna mambo mawili yanaweza kujitokeza, nayo ni kuwa na ndoa iliyojaa matarajio ya watarajiwa (kama yalikuwepo kabla) au kuwa na ndoa iliyokosa matarajio ya watarajiwa na hivyo mwisho wake kuwa ni balaa badala ya raha, dhiki badala ya faraja.

Anaweza mtu kuoa au kuolewa na akafurahia uamuzi wake huo kwa jinsi ndoa ilivyotimiza matakwa ya kuitwa ndoa.

Lakini mwingine akajutia uamuzi wake kutokana na kukithiri maudhi mpaka kufika kuhasimiana na kuachana.

Ili kuepukana na hali hii, kuna haja ya kuwa na utaratibu mahususi kwa wazazi, wazee na viongozi wetu wa dini katika jamii yetu, kujenga mazoea ya kutoa mafunzo na miongozo kwa vijana wetu ili kujaribu kutoa mwongozo kujaribu kuokoa janga hili la kasi ya kuharibika mahusiano ya ndoa, jambo ambalo Mwenyezi Mungu anasema linamchukiza sana.

Kwa mtazamo wangu, dini ndio muongozo namba moja wa kujenga ustaarabu ya maisha ya mwanadamu.

Kwa maana hiyo kuna haja hasa kwa Waislamu, ukiacha zile hutba za ndoa, kusisitizia thamani ya mafunzo ya dini katika kuliendea jambo hili.

Ifahamike tu kwamba msingi wa ndoa yeyote ili iweze kuwa imara, lazima uwe ni mafunzo ya dini.

Dini ndio mwalimu wa maadili, dini ndio mwalimu wa busara, dini ndio mwalimu wa uvumilivu na subra, dini ndio ustaarabu wa maisha, dini ndio chanzo cha kumjua na kumtegemea Mwenyezi Mungu aliyetuumba, ambaye ndiye mwenye dini yake na kaamuru wanadamu kuifuata ili kufaulu hapa duniani na kesho akhera.

Utulivu katika ndoa ni moja katika mambo muhimu yanayodumisha maisha ya ndoa kwa wanandoa.

Vijana wanaotarajia kutimiza suna hiyo wanatakiwa kufundishwa hilo na wawe na yakini na hilo.

Haina maana kosa kidogo tu, au kosa moja likamfanya mtu mara moja akakosa uvumilivu wa kutoa nafasi ya mwenzake kuonywa au kujirekebisha, yeye keshaamua.

Lakini Umuhimu wa ndoa Kwa kuoa wajane, wajakazi, maskini au mafukara, kuleta maana kwamba ndoa kunusu.

“Na waozeni wajane miongoni mwenu na wema katika watumwa wenu na wajakazi wenu”.

Ndoa huunganisha koo kufikia kuweza kurithiana kati ya mume na mke.

Annisaa 12
Ndoa huzuia zinaa.

Katika Hadithi ya Mtume (Saw) amesema,“Enyi vijana mwenye kuweza miongoni mwenu kuoa na aoe kwani (ndoa huleta) kuinamisha macho na kinga kwa utupu na asieweza basi na afunge kwani hiyo ndiyo kinga”.(Bukhari na Muslim).

Aidha amesema katika hadithi yake ,

”Atakapokujieni mtakayemridhia kwa tabia zake na dini yake, basi muozesheni na kama hamkufanya itakuwa fitna katika ardhi na ufisadi mkubwa”. Sahihul Jaamii.

Lakini mahusiano ya ndoa ndiyo starehe ya kipekee isiyobagua, inayomgusa kila mtu katika dunia kwa mume na mke.

Awe tajiri au maskini, mweusi au mweupe nk.

Ni jambo la msingi kwa kila mwana ndoa au anayetarajia kuingia katika ndoa, afahamu kwamba ndoa ni kati ya riziki ambazo Mwenyezi Mungu amewapa waja wake.

Katika ndoa kuna wajibu, haki, majukumu na utaratibu wake katika maisha.

Kabla ya kuoa au kuolewa na kufunga ndoa, kuna haja ya kujiuliza kwanini unaliendea jambo hilo.

Hili ndio swali la kwanza muhusika anapaswa kujiuliza ndani ya moyo wake na kupata majibu yake.

Ndoa humpa mtu heshima katika jamii, kupata watoto,kutafuta stara, kujenga familia bora, kuwaridhia wazazi wawili, kukidhi hamu za kijinsia.

Lakini wapo pia ambao kufikia maamuzi ya kuoa kwakufuata marafiki, kusaidiana majukumu kama vile kupika na kuosha nguo, kusaidia ulezi wa wazazi, kupata mali na utajiri, kuepuka lawama na maudhi nk.

Ni lazima yawepo malengo ya kuoa kabla ya tendo lenyewe.

Lakini malengo yenyewe lazima yawe sahihi na siyo ya kinafsi na ya matamanio tu.

Mtume (saw) amesema, “Mwanamke huolewa kwa mambo manne.

Kwa (ajili ya) mali yake, kwa nasaba yake, kwa uzuri wake na kwa dini yake, basi mtafuteni mwenye dini (kwani) mikono yako itatakatika na michanga.

(Bukhari na Muslim).

Kwa muongozo huo katika Uislamu, unaonekana umuhimu wa kujua lengo kabla ya tendo la kufunga ndoa.

Hii ni kwa kuwa ndoa ni moja ya njia za kuunda jamii, hivyo ni vizuri malengo yakafahamika mapema na yawe katika mtazamo na madhumuni sahihi.

Comments

  1. Aaamin,, hakika kuna haja ya sisi Vijana ambao tuna nia ya kuliendea hili jambo kuwa makini sana. Pia familia zipunguze kuzifanya ndoa kuwa kitega uchumi,, maana inatukatisha tamaa sana

    ReplyDelete
  2. Wynn Palace, Las Vegas (NV) - Jtm Hub
    Wynn Palace offers its 군포 출장안마 guests a 24-hour casino, a casino, luxury 충청북도 출장마사지 dining and 목포 출장안마 a nightlife 계룡 출장안마 experience. Location: 부천 출장샵 Las Vegas (NV). Distance

    ReplyDelete

Post a Comment

Popular posts from this blog

MWANAUME MWENYE MALENGO NA WEWE UTAMTAMBUA KWA HAYA

MAPENZI NA USHIRIKINA